TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

YAHUSU: KUWAPONGEZA IMF KUIPATIA TANZANIA MSAADA ILI KUSAIDIA KUPAMBANA NAATHARI ZA UGONJWA WA CORONA

Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) inalipongeza shirika la Fedha Duniani, IMF kupitia mfuko wake wa ‘Catastrophe Containment and Relief Trust (CCRT)’ kwa uamuzi ulioufikia tarehe 10 Juni 2020 wa kuipatia Tanzania msaada wa dola za Kimarekani milioni 14.3 sawa na bilioni 33 fedha za kitanzania ili kuwezesha  kuhimili athari zitokanazo na janga la ugonjwa wa CORONA katika nyanja za kijamii na kiuchumi.

kwa mujibu wa taarifa  iliyotolewa jijini Washington DC nchini Marekani imesema kuwa Bodi Tendaji ya shirika hilo imefikia uamuzi huo kuwa fedha hizo ambazo Tanzania ilipaswa kulipa sasa zitatoka katika mfuko wa kudhibiti majanga (CCRT) na kuweka unafuu wa kulipa deni. IMF inasema deni hilo lilipaswa kulipwa kati ya sasa na tarehe 13 mwezi Oktoba 2020. Wameongeza pia nyongeza ya msaada mwingine utatolewa kati ya Oktoba 14, 2020 hadi Aprili 13 mwaka 2022 itategemea uwepo wa fedha kwenye mfuko huo.

Msaada huu umekuja kipindi muafaka ambapo COVID-19 imedhoofisha matarajio ya ukuaji uchumi wa Tanzania ambapo sasa inakabiliwa na anguko kubwa la mapato kwenye sekta ya utalii, shinikizo kwenye bajeti na kuanguka kwa ukuaji wa pato la ndani la taifa (GDP), kutoka asilimia 6 hadi asilimia 4 katika mwaka 2020/2021 wa fedha.

 Kwa mujibu wa taarifa za Umoja wa Mataifa ya biashara na maendeleo (UNCTAD) zilizotolea 10 Machi 2020 Geneva Uswisi zinasema “Mgogoro wa kimataifa wa kiafya uliosababishwa na janga la virusi vya Corona au COVID-19 unaweza kuwa na athari kubwa za kiuchumi, na kusababisha upungufu wa dola za Kimarekani bilioni 2,000, pamoja na dola bilioni 200 kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.

Hivi karibuni Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) kupitia vyombo vya habari ilizitaka IMF, Benki ya Dunia (WB) na nchi wakopeshaji duniani kuchukua hatua za haraka na kuipa unafuu mkubwa nchi ya Tanzania kuacha kulipa madeni yake yote kwa sasa na kuipa misaada na mikopo mingine yenye masharti nafuu ili ielekeze nguvu na uwezo wake wote katika kupambana na ugonjwa wa Corona na kuukoa uchumi wake usiingie kwenye mdororo unaoinyemelea kwa haraka sana.

TCDD ilikutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti jijini Dodoma mwezi Aprili 2020 kulitaka Bunge kuishinikiza Serikali kuziomba nchi wakopeshaji kusamehe madeni au kuipatia Tanzania misaada na mikopo yenye masharti nafuu ili kupambana na CORONA. Vile vile TCDD iliwaandikia barua IMF na Benki ya Dunia kuwataka wachukue uamuzi wa kusamehe Tanzania madeni au kutoa misaada na mikopo yenye masharti nafuu ili kuokoa mdororo wa kiuchumi.

TCDD kwa pamoja na serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip  Mpango (MB) alipokuwa akiwasilisha bajeti ya mwaka 2020/2021 bungeni 11 Juni 2020 tunapenda kuipongeza IMF kwa kutoa msaada kwa Tanzania takriban Bilioni 33 fedha za kitanzania ili kuiwezesha kupambana na athari zilizosababishwa na CORONA. Tunasisitiza kuwa IMF wanaendelea kuomba mashirika mengine yatoe msamaha wa madeni, misaada na mikopo yenye masharti nafuu kwa nchi zilizopata athari za ugonjwa huu wa CORONA ili ziweze kujiimarisha kiuchumi. Tanzania inakuwa nchi ya 27 kunufaika na msaada  huo wa madeni kupitia mfuko wa CCRT wa IMF ambapo jumla ya fedha zilizotolewa kuziba pengo la malipo kwa nchi hizo ni dola milioni 243.

Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) ni muunganiko wa asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) zenye malengo ya ufuatiliaji, ushawishi kuhusu bajeti, sera na Deni la Taifa kwa maendeleo ya nchi. TCDD ilisajiliwa mwaka 2007 chini ya sheria ya NGO namba 24 ya mwaka 2002. TCDD imejikita katika ufuatiliaji wa mwenendo wa Deni la Taifa na kutoa ushauri kwa  Bunge na Serikali kuhusu ukopaji wa uwajibikaji kwa maendeleo ya Taifa.  

Hebron Timothy Mwakagenda

Mkurugenzi Mtendaji         

17.06.2020