Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali 2020/21 kuhusu Usimamizi wa Deni la Serikali

Nilibaini Deni la Serikali limefikia Sh. Trilioni 64,519.63 katika mwaka wa fedha 2020/21 ikilinganishwa na Sh. Trilioni 56,756.70 lililoripotiwa mwaka 2019/20. Kuna ongezeko la Sh trilioni 7,762.93 (13.7%) katika mwaka huu ikilinganishwa na Sh. Trilioni 3,652 (7%) kwa mwaka uliopita.

Deni la Serikali linajumuisha Deni la Ndani na Nje la Sh. Trilioni 18,934.61 na Sh. Trilioni 45,585.02 mtawalia kwa mwaka wa fedha 2020/21 ikilinganishwa na Sh. bilioni 15,515 na Sh. Trilioni 41,242 kwa mwaka 2019/20.

Ongezeko hilo limesababishwa na kushuka kwa thamani ya Shilingi na mikopo halisi (mapokezi ya mikopo mipya dhidi ya ulipaji wa mikopo). Nilibaini kuwa, deni la Serikali ni himilivu. Uwiano wa thamani ya sasa ya deni la Serikali (deni la nje na deni la ndani) kwa Pato la Taifa (GDP) umebaki kuwa chini ya kiwango ukomo/elekezi.

 Hata hivyo, nilibaini kuwa vihatarishi vya deni la nje vimeongezeka kutoka kiwango cha chini hadi kufikia kiwango cha wastani. Hii inachangiwa na athari za janga la UVIKO-19 kwenye sekta ya utalii na uchumi wa dunia kwa ujumla.

 Pia, nilibaini uwapo wa mikopo 11 yenye thamani ya Sh. bilioni 2,380 iliyosainiwa kati ya mwaka 1990 na 2020, lakini fedha zake hazikupokelewa hadi tarehe 30 Juni 2021.