Sehemu kubwa ya Bajeti ya 2017/18 inalipia deni la Taifa

July 24, 2017
  • Kwa mwaka huu wa fedha, Sh9 trilioni sawa na asilimia 28 ya bajeti zitatumika kwa ajili ya kulipa deni la Taifa.

By Prof Honest Ngowi Pngowi2002@yahoo.com

Deni la Taifa ni kati ya mambo muhimu katika uchumi wa Tanzania. Kuna mambo mengi ambayo hayafahamiki kwa watu wengi licha ya kwamba kiwango kikubwa cha bajeti mwaka huu kitatumika kulipa deni hili.

Kwa mwaka huu wa fedha, Sh9 trilioni sawa na asilimia 28 ya bajeti zitatumika kwa ajili ya kulipa deni la Taifa.

Deni la Taifa ni fedha ambazo nchi inadaiwa na wadeni wa ndani na nje likijumuisha sekta binafsi na ya umma yaani Serikali. Kwa kawaida deni la Serikali ni kubwa kuliko la sekta binafsi.

Deni la ndani ni fedha ambazo zilizokopwa kutoka vyanzo vya ndani ya nchi wakati la nje linatokana na mikopo kutoka taasisi na mamlaka za kimataifa. Mkopo unaochangia deni la Taifa huweza kuwa wa masharti nafuu au wa biashara.

Ule wa masharti nafuu huwa na riba ndogo na kipindi kirefu cha ulipaji, kikiwamo kipindi cha msamaha kabla ya kuanza kulipa. Mikopo ya biashara hutozwa riba kubwa na pengine kulipwa kwa muda mfupi. Serikali hukopa kwa kutokuwa na mapato ya kutosha kukidhi bidhaa na huduma za umma.

Deni zuri

Deni la Taifa siyo jambo baya iwapo mkopo utatumika kwa shughuli za maendeleo. Shughuli hizi ni pamoja na ujenzi wa miundombinu inayotakiwa kuchochea maendeleo ya uchumi na kuzalisha mali kama vile barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na mawasiliano kama ya simu.

Shughuli nyingine za maendeleo ni uwekezaji katika rasilimali watu kupitia elimu na afya katika upana wake. Kusudi mkopo uwe na maana zaidi ni vizuri uwekezaji huu ukafanywa kwa kiwango kikubwa na rasilimali watu na malighafi kutoka ndani.

Mkopo wa kujenga miundombinu huwa na maana zaidi kiuchumi kama kampuni za ndani ndizo zitajenga miundombinu husika. Maana yake ni kuwa nchi hufaidika zaidi kwa kutumia kampuni zake kutekeleza miradi inayogharamiwa kwa mikopo, badala ya kutumia kampuni za nje ya nchi.

Kampuni za kizawa hubakiza sehemu kubwa ya fedha ndani ya nchi na kuchochea shughuli za uchumi na biashara. Changamoto huweza kuwa masharti ya mikopo hii na uwezo wa kutosha wa kampuni za ndani.

Pia, deni huwa zuri kiuchumi kama linaleta thamani ya fedha iliyokopwa na faida zake kufikia wadau wengi.

Deni baya

Uzuri au ubaya wa deni la Taifa ni namna linavyotumiwa. Kama deni likitumika kugharamia matumizi ya kawaida badala ya kutekeleza miradi ya maendeleo huwa baya kwa uchumi wa nchi.

Matumizi ya kawaida uhusisha vitu kama safari, mikutano, uendeshaji wa kila siku wa ofisi kama kulipa mishahara. Pia, deni kubwa la Taifa ni mzigo na baya kiuchumi.

Hii ni kwa sababu, deni la Taifa hulipwa pamoja na riba. Riba huwa ni asilimia fulani ya deni lote. Hivyo, gharama ya kulipa deni inategemea ukubwa wa deni na riba inayolipwa. Kutegemea aina ya mkataba, nchi huweza kulipa riba tu kwa muda fulani au kulipa deni na riba kwa wakati mmoja.

Pale deni linapolipwa maana yake ni kuwa nchi inaacha kutumia fedha zinazolipa deni hilo kwa shughuli nyingine, kama kujenga miundombinu na kutoa huduma za jamii kama elimu, afya na maji.

Ukubwa wa deni

Deni la Taifa likiwa kubwa husababisha gharama ya kukopa kuwa kubwa zaidi. Hii ni kwa sababu nchi yenye deni kubwa uwezo wake wa kulipa huwa mdogo.

Hivyo, wakopeshaji huwa na wasiwasi kuhusu uwezekano wa kulipwa. Kuna kampuni kubwa duniani ambazo hutoa maoni yao kwa wakopeshaji kuhusu hali ya nchi kukopesheka au kutokopesheka.

Kampuni hizo ni Moody’s, Standard & Poor’s na Fitch Ratings. Kama deni la nchi ni kubwa na ubebekaji na uhimilivu wake ni mgumu, kampuni hizi huipa alama ndogo hivyo kuifanya isikopesheke kwa urahisi na inapokopesheka riba huwa juu sana.

Nchi isipolipa deni kwa kiwango na muda uliokubaliwa huweza kuadhibiwa na wakopeshaji. Adhabu huweza kuwa kuongezeka kwa riba. Hata hivyo, masoko ya fedha yanayokopesha nchi huweza kutoa adhabu kali kuliko kuongeza riba.

Hii ni pamoja na kuitangaza nchi husika na kuiweka katika kundi la nchi zisizokopesheka. Ndiyo maana ni muhimu kulipa deni la Taifa kwa wakati na kiwango kilichokubalika ili kuepuka adhabu kutoka kwa wakopeshaji.

Sarafu

Duniani kuna wakopeshaji wengi wanaotumia sarafu za aina mbalimbali kama Euro, Dola, Pauni, Yuan na nyinginezo. Hata hivyo, mapato ya Tanzania ambayo hutumika kulipa deni la Taifa kwa kiwango kikubwa yapo katika Shilingi.

Maana yake kiuchumi, ni kuwa, ikiwa Shilingi inapoteza thamani kulinganisha na fedha za kigeni tulizokopea, (mara nyingi huwa Dola ya Marekani) tutahitaji Shilingi nyingi zaidi kulipa deni lilelile bila hata kukopa zaidi. Hivyo ni muhimu kuimarisha Shilingi kwa njia mbalimbali.

Njia kuu na nzuri zaidi ya kiuchumi ya kuimarisha sarafu ya nchi ni kuuza bidhaa na huduma nje ya nchi kwa wingi na kimkakati; kuvutia uwekezaji utakaoongeza fedha za kigeni; kupokea misaada ya fedha za kigeni hata fedha kutoka kwa diaspora.

Haya ni baadhi tuu ya mambo ya msingi katika deni la Taifa ambao Watanzania wanapaswa kufahamu. Mwisho wa siku ndiyo wanaopaswa kunufaika na kulipa deni hili kwa njia mbalimbali.

Mojawapo ni kupitia kodi na nyingine ni kwa kukosa baadhi ya bidhaa na huduma za umma katika wingi na ubora unaotakiwa. Hii hutokea pale fedha za kugharamia mambo haya zinapotumika kulipa deni la Taifa. Wote tukilipa kodi tutapunguza haja ya Serikali kukopa.