YALIYOPENDEKEZWA KWENYE MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2017/18, KUHUSU DENI LA TAIFA

June 15, 2017

HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), AKIWASILISHA BUNGENI

08 Juni, 2017  Dodoma

Deni la Taifa

  1. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia Deni la Taifa kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada SURA 134. Ili kuhakikisha kuwa deni la Taifa linaendelea kusimamiwa ipasavyo, Bunge lako Tukufu lilipitisha marekebisho ya Sheria hiyo mwezi Novemba, 2016. Baadhi ya maeneo yaliyorekebishwa ni pamoja na: kuongeza masharti kwa Taasisi na Mashirika ya Umma yanayoomba dhamana ya Serikali ili kudhibiti utoaji wa dhamana hizo; kuweka utaratibu maalum wa kisheria ambao unahakikisha kwamba fedha zilizokopwa na Serikali ya Muungano kwa lengo la kugharamia miradi ya maendeleo Zanzibar inafika kama ilivyokusudiwa; na kuongeza wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Kamati ya Kitaifa ya Kusimamia Deni la Taifa.
  2. Mheshimiwa Spika, Hadi Machi 2017, deni la Taifa lilifikia shilingi bilioni 50,806.5. Kati ya kiasi hicho, deni la Serikali ni shilingi bilioni 42,883.6 na deni la sekta binafsi ni shilingi bilioni 7,922.9. Deni la Serikali limeongezeka kwa asilimia 9.2 kutoka shilingi bilioni 39,274.6 Machi, 2016 hadi shilingi bilioni 42,883.6 Machi, 2017. Ongezeko la deni la Serikali lilitokana na mikopo mipya na ya zamani iliyopokelewa katika kipindi cha mwaka 2016/17 kutoka vyanzo vya masharti nafuu na ya kibiashara, malimbikizo ya riba ya deni la nje kwenye nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris ambazo zinatakiwa kutoa msamaha wa madeni lakini bado hazijatoa pamoja na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola za Marekani.
  1. Mheshimiwa Spika, deni la Serikali linajumuisha deni la ndani la shilingi bilioni 12,073.7 sawa na asimilia 28.1 na deni la nje la shilingi bilioni 30,809.9 sawa na asilimia 71.9. Deni la nje linajumuisha mikopo ya masharti nafuu kutoka kwenye mashirika ya fedha ya kimataifa, sawa na asilimia 56.8, mikopo kutoka nchi wahisani ilifikia asilimia 16.3 na mikopo kutoka mabenki ya kibiashara ya kimataifa ilifikia asilimia 26.9 ya deni lote la nje. Mikopo hiyo ilitumika kugharamia miradi ya maendeleo hususan katika sekta za ujenzi (barabara na reli), nishati, uchukuzi, elimu na maji.

Tathmini ya Uhimilivu wa Deni la Taifa

  1. Mheshimiwa Spika, matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika mwezi Novemba, 2016 yalibainisha kuwa Deni la Taifa ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu. Katika tathmini hiyo, viashiria vinaonesha kuwa: thamani ya sasa ya jumla ya Deni la Taifa (Present Value of Total Public Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 34.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 56; thamani ya sasa ya Deni la nje (Present Value of External Debt) kwa Pato la Taifa ni asilimia 19.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 40; thamani ya sasa ya deni la nje kwa mauzo ya nje ni asilimia 97.7 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 150; na thamani ya sasa ya deni la nje kwa mapato ya ndani ni asilimia 145.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia
  1. Viashiria hivyo vinapima uwezo wa nchi kukopa bila kuathiri uhimilivu wa deni (solvency indicators).
  1. Mheshimiwa Spika, kutokana na tathmini ya uhimilivu wa deni la Taifa, ambayo inapima uwezo wa nchi kulipa deni, uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani umefikia asilimia 11.5 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 20 na uwiano wa ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 7.8 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia
  1. Kwa kuzingatia viashiria hivyo, ambavyo vipo chini ya ukomo unaokubalika kimataifa, Tanzania bado ina uwezo wa kuendelea kukopa kutoka ndani na nje ya nchi ili kugharamia shughuli zake za maendeleo na pia ina uwezo wa kulipa mikopo inayoiva kwa kutumia mapato yake ya ndani na nje.