Mapato hayakukidhi, Deni la Taifa laongezeka.

Dar es Salaam. Kati ya Sh 29.5 trilioni iliyoridhiwa kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, ripoti ya Bank Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha ni Sh19.65 trilioni zilitumika.

Kutoka kwenye vyanzo mbalimbali vya serikali haikukamilisha lengo la kukusanya kiasi kilichoainishwa, BoT inasema ilikusanya Sh16.63 trilioni ambazo ni pungufu kwa zaidi ya Sh12 trilioni. Kutokana na upungufu wa mapato halisi yaliyopatikana dhidi ya matumizi ya msingi ambayo yalikuwa hayakwepeki, serikali illazimka kukopa kutoka vyanzo vya ndani na nje.

Matumizi

Baada ya kuanisha vipaumbele vitakavyosaidia kukuza uchumi na kupunguza umaskini, serikali ilieliekeza fedha chache ilizonazo kwenye maeneo muhimu.

Kutokana na ukweli huo, ilitumia Sh19.65 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 18.4 ya Pato la Taifa kwa mwaka uliopita wa fedha. Kati ya fedha hizo matumizi ya kawaida yalikuwa Sh12.26 trilioni na miradi ya maendeleo Sh7.39 trilioni

“Asilimia 69.6 ya miradi ya maendeleo ilitekelezwa kwa fedha za ndani. Miradi ya maendeleo ilikuwa sawa na asilimia 37 ya matumizi yote,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Kwenye matumizi hayo, ripoti serikali ilipungukiwa Sh1.59 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 1.5 ya Pato la Taifa hivyo kulazimika kukopa hasa kutoka vyanzo vya nje ya nchi.

Kufanikisha hilo, serikali ilikopa Sh1.7 trilioni huku ikitoa Sh110.9 bilioni kulipa deni la ndani.

Kwenye matumizi hayo, serikali ilizingatia utekelezaji wa mpango wa maendeleo kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa viwanda na yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Ripoti inasema, miongoni mwa yaliyofanywa ni kukamilisha utekelezaji wa baadhi ya miradi mikubwa hasa usambazaji wa umeme vijijini, mpango wa maji vijijini na utoaji wa elimu bure.

Vilevile, serikali ilimaanisha ukusanyaji wa mapato hasa yatokanayo na kodi na kudhibiti matumizi.

“Bajeti ilikabiliwa na nakisi hasa mkopo kutoka kwa mashirika ya kimataifa na misaada kutoka nchi wahisani.”inasema ripoti hiyo.

Mapato

Mikakati ya serikali kudhibiti upotevu na kuimarisha vyanzo vilivyopo umeongeza ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 19.7 mwaka uliopita na kufika Sh16.63 trilioni.

Mapato hayo yalikuwa sawa na asilimia 15.6 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 14.3 za mwaka wa fedha 2015/16.

Katika kiasi hicho, mapato yatokanayo na kodi yalikuwa Sh14.05 trilioni ambayo ni sawa na asilimia 13.1 ya pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 12.8 za mwaka 2015/16.

Mapato yasiyotokana na kodi yalikuwa Sh2.07 trilioni au asilimia 1.9 ya Pato la Taifa. Serikali ilipokea msaada wa Sh912 bilioni huku washiriki wa maendeleo wakichangia Sh120.6 bilioni wakizielekeza kwenye miradi ya maendeleo.

Deni la Taifa

Licha ya kuongezeka kwa asilimia 9.1 kwa mwaka uliopita, ripoti inasema deni la Dola 23.77 bilioni (zaidi ya Sh52.29 trilioni) baado ni vumilivu. Deni hilo ambalo ni sawa na asilimia 48.9 ya pato la Taifa, tipoti inasema “Ni himilivu kwa viwango vyote vya kimataifa.”

Tathmini ya uhimilivu wa Deni la Taifa (DSA) iliyofanywa na  Shirika la Fedha Duniani (IMF) mwaka 2016 ilibainisha kuwa bado Tanzania inakopesheka. Shirika hilo liliweka wazi kuwa kiwango cha juu cha Deni la Taifa kuwa ni asilimia 56 ya Pato la Taifa kiasi ambacho Tanzania bado haijafikia hata leo.

Katika deni hilo, Dola 18.49 bilioni (zaidi ya Sh40.67 trilioni) lilikwa la nje na Dola 5.28 bilioni (zaidi ya Sh11.78 trilioni) lilikuwa la ndani.

Kwa mwaka huo, Dola 854.2 milioni (zaidi ya Sh1.87 trilioni) zilitumika kulipa deni la Taifa lililoongezeka kutoka Dola 21 bilioni (zaidi ya Sh46.2 trilioni) lililokuwa hapo Juni, 2016.

Mpaka Juni mwaka jana, deni la ndani, Sh11.78 trilioni, lilikuwa limeongezeka kwa Sh1.77 trilioni ndani ya miezi 12 ya utekelezaji wa hiyo.

Katika muda huo, kwa kutumia amana zake, serikali ilikopa Sh6.94 trilioni ikiwa ni ongezeko la tatribani Sh500 bilioni ya lengo la kukopa Sh6.49 trilioni.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi, Jumanne, Januari 16,2018