Kila Mtanzania sasa adaiwa milioni moja

Raia Mwema (Mwandishi Wetu)

Toleo la 463

22 Jun 2016

 

DENI la Taifa limepaa na kufikia dola za Marekani bilioni 20.5 (Shilingi trilioni 44.7) hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu, kutoka dola bilioni 19.1 (Shilingi trilioni 38) mwezi Juni, mwaka jana.
Kwa kiasi hicho cha fedha, kama utagawanya deni hilo kwa idadi ya Watanzania ambao sasa wanakadiriwa kufikia milioni 45, kila Mtanzania sasa anadaiwa kiasi cha shilingi milioni moja.
Kwa mujibu wa muhtasari wa sera ya fedha kwa kipindi cha kuanzia mwezi Juni mwaka huu uliotolewa wiki iliyopita na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ongezeko la deni la taifa ni linatokana na uchukuaji wa mikopo mipya pamoja na malimbikizo ya riba za mikopo ya awali.
Kiasi cha fedha zilizokopwa na Tanzania kwa mwezi wa Aprili mwaka huu ni dola za Marekani bilioni moja (Shilingi trilioni mbili). Kiasi kikubwa cha mikopo hiyo kilikopwa na serikali, huku sekta binafsi ilikopa kiasi kidogo.
Lakini kitabu cha hali ya uchumi ya mwaka 2015 kilichotolewa na 0fisi ya Takwimu Nchini (NBS) kimeonyesha kwamba hadi kufikia mwishoni mwa Machi 2016, Deni la Taifa lilifikia shilingi bilioni 45,443.21 ikilinganishwa na shilingi bilioni 35,010.4 Machi 2015, sawa na ongezeko la asilimia 29.8.
Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 38,826.5 lilikuwa deni la Serikali na shilingi bilioni 6,592.3 lilikuwa deni la sekta binafsi.
Hii ilitokana na kuongezeka kwa mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Kimarekani na malimbikizo ya riba kwa mikopo ya nje kwa nchi zinazotakiwa kutoa msamaha wa madeni kwa mujibu wa Paris Club lakini bado hazijatoa.
Hata hivyo, tathmini ya uhimilivu wa Deni la Taifa iliyofanyika Septemba 2015 ilionesha kuwa deni la Taifa ni himilivu.
Viashiria vya deni vinaonesha kuwa: thamani ya deni la nje kwa Pato la Taifa ilikuwa asilimia 20.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 50; thamani ya deni la nje kwa mauzo ya nje ilikuwa asilimia 104.4 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 200.
Thamani ya deni la nje kwa mapato ya ndani ilikuwa asilimia 157.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 300; na ulipaji wa deni la nje kwa kutumia mapato ya ndani ulifikia asilimia 13 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 22.
Deni la Taifa la nje lilikuwa Dola za Marekani milioni 15,435.3 Machi 2016 ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 14,265.00 Desemba 2014, sawa na ongezeko la asilimia 13.3. Kati ya kiasi hicho, Dola za Marekani milioni 13,158.78 zilikuwa ni deni la Serikali na Dola milioni 3,009.59 zilikuwa ni deni la sekta binafsi.
Kuongezeka kwa deni kulitokana na kupatikana kwa mikopo mipya kwa ajili ya miradi ya maendeleo na malimbikizo ya riba kwa nchi ambazo siyo mwanachama wa kundi la Paris.
Mchanganuo wa deni la nje la Serikali kwa wakopeshaji unaonesha kwamba wakopeshaji wakubwa ni mashirika ya fedha ya kimataifa.
Hadi kufikia Machi 2016 mashirika ya fedha ya kimataifa yalichangia asilimia 56.5 ikilinganishwa na asilimia 57 Machi 2015; Mikopo yenye masharti ya kibiashara ilichangia asilimia 29.2; na mikopo kutoka nchi wahisani ilichangia asilimia 13.2 ya mikopo yote ya nje.
Kutokana na masharti, gharama na ugumu wa upatikanaji mikopo yenye masharti ya kibiashara, Serikali imedhamiria kuendelea kukopa kutoka kwenye vyanzo nafuu na kuhakikisha kuwa mikopo yenye masharti ya kibiashara inatumika kugharamia miradi ya maendeleo inayochochea kwa kasi ukuaji wa uchumi.
Deni la ndani liliongezeka kwa asilimia 6.9 kutoka shilingi bilioni 9,376.85 Machi 2014 hadi kufikia shilingi bilioni 10,027.34 Machi 2016.
Deni hili linajumuisha dhamana za Serikali za muda mfupi kwa ajili ya kudhibiti mfumuko wa bei kwenye uchumi kiasi cha shilingi bilioni 24.42. Ongezeko la deni la ndani lilitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya Serikali kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Uchambuzi unaonesha kuwa, hadi kufikia Machi 2016, Hati Fungani (Treasury Bonds) zilifikia shilingi bilioni 4,599.95 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi bilioni 4,006.22 Machi, 2015 ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.8.
Aidha, dhamana za muda mfupi ziliongezeka kutoka shilingi bilioni 1,588.47 Desemba 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 2,889.27 Machi 2016; Hati Fungani maalumu zilipungua kutoka shilingi bilioni 1,479.30 Machi, 2015 hadi kufikia bilioni 1,465.43 Machi,2016; dhamana za muda mfupi kwa ajili ya kuondoa ujazi wa fedha kwenye uchumi zilipungua kutoka shilingi bilioni 1,131.97 Machi, 2015 hadi shilingi bilioni 24.42 Machi 2016.
Uchambuzi wa deni la ndani la Serikali kwa makundi yanayohodhi ulibainisha kuwa benki za biashara zinahodhi sehemu kubwa ya deni hilo. Hadi kufikia Machi 2016, benki za biashara zilikuwa zinahodhi asilimia 48.7 ya deni la ndani.
Hii imechangiwa na kukua kwa sekta za benki nchini pamoja na kuwepo kwa athari ndogo za kuikopesha serikali ikilinganishwa na sekta binafsi.
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na mashirika ya bima ni ya pili kwa kuhodhi asilimia 24.5, ikifuatiwa na Benki Kuu ya Tanzania asilimia 19.3 na watu binafsi na mashirika madogo asilimia 7