Kamati ya Bajeti yaishauri Serikali kujitathmini ulipaji Madeni

By Sharon Sauwa, Mwananchi ssauwa@mwananchi.co.tz  Tuesday, November 6, 2018

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Bajeti imeishauri Serikali kujipima na kuweka ukomo kwenye uwiano wa ulipaji wa deni la Serikali na mapato ya ndani ili kuona athari yake kiuchumi na kibajeti.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Bungeni Novemba 6, 2018 na mwenyekiti wa kamati hiyo, George Simbachawene wakati akisoma taarifa ya kamati hiyo kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa pamoja na mwongozo wa kutayarisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Amesema deni la Serikali limeendelea kukua kutoka Dola za kimarekani milioni 21,623.26 ( Juni mwaka 2017) hadi Dola za Marekani Milioni  23,234.26 ( Juni mwaka 2018).

Amesema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 39.4 ya Pato la Taifa na kwamba hilo limetokana na Serikali kuendelea kukopa kwa ajili ya kugharamia bajeti ya Serikali.

“Kwa maelezo ya Serikali deni letu linaonekana ni himilivu. Hata hivyo, kamati inaishauri Serikali ijipime na kuweka ukomo kwenye uwiano wa ulipaji wa deni na mapato ya ndani ili kuona athari yake kiuchumi na kibajeti,” amesema.

CHANZO GAZETI LA MWANANCHI