Dodoma Kuwa Kama Ulaya Baada Ya Benki Ya Maendeleo Ya Afrika Kutoa Mkopo Wa Sh. Bilioni 414 Kujenga Barabara Za Mzunguko
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
Jiji la Dodoma na vitongoji vyake, hivi karibuni litabadilika
mwonekano wake na kuwa la viwango vya kimataifa baada ya Benki ya Maendeleo ya
Afrika, AfDB kuipatia Tanzania mikopo yenye masharti nafuu ya dola milioni 180
sawa na shilingi bilioni 414 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za pete (ring
road) kwa kiwango cha lami na uboreshaji wa miundombinu katika Jiji hilo.
Makubaliano ya mikopo hiyo yametiwa saini Jijini Dar es
Salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James, kwa
upande wa Serikali, na Meneja Mkazi wa Benki hiyo hapa nchini, Bw. Alex Mubiru.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mikopo hiyo, Bw.
Doto James, amefafanua kuwa mradi utahusisha Ujenzi wa barabara ya mzunguko wa
njia nne zenye urefu wa km 110.2 kwa kiwango cha lami kutoka Nala – Veyula –
Ihumwa – Matumbulu.
Alisema mikopo hiyo pia inahusisha uboreshaji wa upatikanaji
wa miundombinu ya huduma za kijamii ikiwemo huduma za maji na vituo vya afya;
Ukarabati wa barabara za mchepuko; na Utekelezaji wa mikakati ya usalama wa
barabarani katika mji wa Dodoma itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka miwili”
alifafanua Bw. James
”Kupitia Mikataba hii, Benki ya Maendeleo ya Afrika itatoa
kiasi cha dola za Marekani milioni 138 kupitia dirisha la Benki ya Maendeleo ya
Afrika (ADB Window) na dola za Marekani milioni 42 zitatolewa kupitia mfuko wa
Africa Growing Together Fund (Mfuko wa Serikali ya China unaosimamiwa na Benki
ya Maendeleo ya Afrika)” alisisitiza Bw. James
Aliishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kuendelea kuunga
mkono juhudi za Serikali za uwekezaji katika miundombinu ya usafiri itakayoiwezesha
Tanzania kufikia azma yake ya kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji katika
Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.
“Uwekaji saini wa Mikataba hii miwili itaongeza kiasi cha
fedha ambacho kimetengwa na Benki kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa barabara
nchini Tanzania, kutoka dola za Marekani milioni 858.16 hadi dola za Marekani
bilioni 1.038, sawa na takribani sh. trilioni 2.39”, aliongeza Bw. James
Alisema Barabara hiyo inaungana na barabara ya Cape hadi
Cairo inayojulikana kama the Great North Road Highway yenye urefu wa km 10,228
inayopita katika nchi nane ambazo ni Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Zambia,
Tanzania, Kenya, Ethiopia, Sudan na Misri na ni barabara ya ukanda wa kati
(central corridor) inayounganisha Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Uganda.
Alidokeza pia kuwa Benki hiyo ya Maendeleo ya Afrika (AfDB),
imeonesha utayari wa kufadhili ukarabati wa barabara ya
Bagamoyo–Pangani-Tanga kwa kiwango cha lami na Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa-Msalato, utakaojengwa mkoani Dodoma ambapo tayari maandalizi
yameanza.
Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika(AfDB), Bw. Alex Mubiru, alisema kukamilika kwa mradi huo kutaiunganisha
Dodoma na mikoa mingine ikiwemo Arusha, Iringa, Singida, na Dar es salaam na
kwamba utasaidia kupunguza msongamano wa magari katikati ya Jiji la Dodoma kwa
sababu magari yanayokwenda kwenye maeneo hayo yatapita pembezoni mwa Jiji.
“Benki ya Maendeleo ya Afrika pamoja na washirika wake
tutatoa asilimia 84 ya gharama za mradi ambazo ni dola za Marekani Milioni 215
wakati Tanzania itatoa asilimia 16 na baadae mwaka huu tutatoa kiasi kingine
cha msaada wa takriban dola milioni 7.2 ambazo zitatumika kwa ajili ya
kuimarisha mazingira kwa kupanda miti kwenye eneo la mradi” alisema Bw. Mubiru.
Aliongeza kuwa hivi sasa Benki yake inajiandaa kutoa mkopo
kwa ajili ya miradi miwili muhimu ukiwemo mradi wa uboreshaji wa barabara
kutoka Bagamoyo-Pangani-Tanga-Horohoro/lunga, Lunga – Mombasa-Malindi pamoja na
ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa-Msalato, miradi ambayo Bodi ya Benki
hiyo inatarajia kuipitisha mwishoni mwa mwaka 2019.
Meneja Mkazi huyo wa AfDB nchini alisema matukio haya yote
yanatokea kwa sababu Benki yake ina imani na kupongeza mafanikio makubwa ya
Serikali ya Tanzania katika kuimarisha maendeleo ya watu wake na kwamba Benki
hiyo iko tayari kuhakikisha azma hiyo inafikiwa.