IMF kuipatia Tanzania fedha ili kukabili athari za Corona

Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeahidi kuipatia Tanzania fedha itakayoihitaji ili iweze kuendelea kukabiliana na athari zitokanazo na janga la Covid 19 kwa ajili ya kuimarisha uchumi wake.

Mkurugenzi Mkazi wa IMF nchini Tanzania Jens Reinke ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamamba John Kabudi katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam.

Reinke ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua madhubuti inazozichukua  katika kukabiliana na janga la Covid 19 ili kuepusha madhara ya kiuchumi na kijamii.

Mazungumzo hayo pia yamelenga miradi ya maendeleo, msamaha wa madeni kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, ushirikiano baina ya IFM na Tanzania, biasara na utalii.

Kwa upande wake, Prof. Kabudi ameishukuru (IMF) kwa msamaha wa madeni ambao umetolewa kwa Tanzania na nchi nyingine, fedha zitakazoziwezesha nchi hizo kuendelea kukabiliana na Covid 19. “Tumeongelea mambo mbalimbali yanayohusu ushirikiano hasa katika kuimarisha uchumi wetu baada ya janga la covid 19, usirikiano kati ya Tanzania na IMF unafahamika na tumekubaliana baadhi ya mambo ambayo tutayafanyia kazi kwa kina ili tuweze kuimarisha uchumi wetu baada ya corona hasa katika sekta ya utalii, biashara na miundombinu,” amesema Prof. Kabudi