Serikali yahakiki deni la Trilioni 2 mifuko ya jamii

Friday, May 4, 2018

By Habel Chidawali, Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

Kwa ufupi

Uhakiki wa deni la mifuko hiyo ulifanyika mwaka 2016 na Serikali ilianza kulipa kwa kutumia hati fungani zinazotarajia kuiva kati ya miaka mitatu (3)

Dodoma. Jumla ya deni lililowasilishwa serikalini kwa ajili ya uhakiki kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii hadi mwaka 2016 ni Sh 2.1 trilioni na deni lililokubaliwa kulipwa ni Sh 1.2 trilioni

Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji ameliambia Bunge kuwa mwaka 2016 Serikali ilifanya uhakiki wa deni la mifuko ya hifadhi ya jamii lililotokana na mikopo ya uwekezaji kwenye miradi mbalimbali ili kuandaa utaratibu wa malipo.

Dk Kijaji amesema baada ya uhakiki kukamilika, Serikali ilianza utaratibu wa kulipa deni hilo kwa kutumia hati fungani maalumu zilizotarajia kuiva ndani ya miaka mitatu na 20

Alikuwa akijibu swali la msingi la Rashid Ali Abdallah (Tumbe-Cuf), ambaye alitaka kujua Serikali imefanya juhudi gani kurejesha mikopo ambayo ilikopa katika mifuko ya LAPF, PSPF, PPF, NSSF, na NHIF.

Naibu Waziri amesema wakati Serikali inaandaa hati fungani ilipendekeza Bunge kuridhia mapendekezo ya Serikali ya kuunganisha mifuko ya pensheni na kuunda mifuko miwili.

“Hatua hiyo ilisababisha Serikali kusitisha zoezi la kuandaa na kutoa hati fungani maalumu hadi hapo taratibu za kuunganisha mifuko ya pensheni zitakapokamilika,” amesema Kijaji.

Chanzo: www.facebook.com/mwananchiNews