Benki ya Dunia kuikopesha Tanzania zaidi ya Tsh. Trilioni 3.9
Source: JamiiForums.
Benki ya Dunia (WB)
imesema ipo tayari kuipaTanzania mkopo wa masharti nafuu wa Dola 1.7 bilioni
ambazo ni zaidi ya Sh3.9 trilioni.
Fedha hizo ni zile zilizobaki katika fungu awamu ya 18 ya
mgao wa chama cha kimataifa cha maendeleo (IDA) kilichopo ndani ya WB ambacho
hujihusisha na kuzisaidia nchi masikini zaidi duniani kupambana na umasikini.
Leo Jumatano Agosti 21, 2019 mkurugenzi mtendaji wa WB
anayesimamia nchi 22 zilizoko Kanda ya Afrika, Anne Kabagambe amemueleza Waziri
wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dk Philip Mpango kuwa kiasi hicho cha fedha
kinatarajiwa kutolewa kabla ya kuanza mgao mpya wa 19 wa IDA utakaoanza Julai
2020.
Kabagambe ambaye yupo nchini kwa ziara ya kikazi amesema
fedha hizo zitatolewa mara baada ya kukamilisha taratibu zote za upatikanaji
wake.
”Fedha hizi zitaelekezwa katika kutekeleza miradi kadhaa
muhimu ikiwemo ya elimu, afya, mradi wa kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (Tasaf) awamu ya pili na uendelezaji wa miji na masuala ya
uchumi jumuishi Zanzibar,” amesema Kabagambe
Taarifa iliyotolewa na wizara ya fedha imeeleza Kabagambe
amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupiga vita
rushwa na ufisadi pamoja na kutekeleza miradi ya jamii ikiwemo reli na kufua
umeme.
Kwa upande wake, Dk Mpango ameiomba benki hiyo kuisaidia
Serikali kwa kuipatia fedha za kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo ya umeme,
reli, maji safi na salama, kuimarisha sekta ya kilimo, viwanda, bandari,
rasilimali watu na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Amesema miradi hiyo itachochea zaidi ukuaji wa uchumi na
kupunguza umasikini wa wananchi kwa kuwa nishati ya umeme itachochea ukuaji wa
sekta ya viwanda hivyo na kukuza ajira, na reli itaimarisha sekta ya usafiri na
uchukuzi